Haki miliki ya picha Getty Images Image caption Waziri wa Rwanda anayehusika na masuala ya Jumuiya ya afrika mashariki Olivier Nduhungirehe

Rwanda imekanusha madai kwamba majeshi yake yameshambulia Burundi.

Waziri wa Rwanda anayehusika na masuala ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, Olivier Nduhungirehe amesema madai ya Burundi hayana msingi wowote na kuongeza kwama yanalenga kufunika matatizo yake ya ndani.

''Tumezoea madai kama hayo kutoka Burundi...kwa miaka kama minne iliyopita wanatushutumu mambo mengi yanayohusiana na usalama mdogo na matatizo ya kisiasa nchini mwao.

Si jambo lililotushangaza hata kidogo, waliandikia jumuiya ya kimataifa na Jumuiya ya kikanda kwamba Rwanda ilivamia Burundi lakini hawakutoa ushahidi wowote wa madai yao.

Madai yao yanalenga kuzubaisha ulimwengu''

  • Mashambulizi dhidi ya maeneo ya jeshi ya Rwanda na Burundi ni kisasi?

Wiki iliyopita Serikali ya Burundi iliishtumu Rwanda kuhusika na shambulio la kijeshi katika mkoa wa Cibitoke kaskazini mwa Burundi.

Waziri Nduhungirehe amesema Burundi inalenga kupotosha dunia kuhusu kuunga kwake mkono makundi ya waasi dhidi ya Rwanda hususan kundi la FLN lililojigamba kuhusika na mashambulio dhidi ya Rwanda karibu na mpaka wa Burundi mwezi uliopita.

Image caption Burundi na Rwanda zimekuwa zikishutumiana kuharibu hali ya usalama ya nchi zao

Mashambulio hayo yalifuatiwa na shambulio lililofanywa katika wilaya ya Mabayi mkoa wa Cibitoke kaskazini mwa Burundi.

Msemaji wa serikali ya Burundi, Prosper Ntahorwamiye aliishutumu Rwanda akisema ushahidi uliopo ni kwamba shambulio dhidi ya Burundi lilifanywa kwa ustadi na kwa kutumia silaha za hali ya juu.

Wakati huohuo bwana Ntahorwamiye ameonya ikiwa Jumuiya za kimataifa na Jumuia za kikanda hazitaingilia kati mzozo huo, Burundi itachukua hatua kali.

Kwa upande wake Rwanda kupitia waziri wake wa masuala ya Jumuiya ya Afrika mashariki imesema haitiwi wasi wasi na onyo hilo la Burundi.

''Hatuna wasiwasi, sisi tunaunga mkono juhudi za amani katika ukanda huu, matatizo ya Burundi ni masuala ya ndani japo Jumuiya ya Afrika mashariki inajaribu kupatanisha.

Sisi matatizo yao hayatuhusu, tunachosema tu ni kwamba tuko tayari kuishi na Burundi kwa amani kama wata-tatua matatizo yao bila kuhusisha Rwanda.

Ila tuko tayari kulinda hadhi ya taifa letu'' alisema waziri Olivier Nduhungirehe.

Haki miliki ya picha Getty Images Image caption Wanajeshi wa Burundi

Mtazamo wa Burundi kuhusu Rwanda

Burundi imekuwa ikidai kwamba Rwanda iliwafadhili waliohusika na kwamba inatoa hifadhi kwao.

Rwanda mara kwa mara imekuwa ikikanusha tuhuma hizo.

Mwaka uliopita Rais Nkurunziza alimwandikia barua rais wa Uganda Yoweri Museveni akiwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika mashariki mwaka huo akisema 'Rwanda sasa si mshirika tena ndani ya Jumuiya bali ni kama adui'.

"Rwanda ndiyo nchi pekee katika kanda hii ambayo ndiyo moja wa wahusika wakuu katika kuvuruga uthabiti wa taifa langu na kwa hivyo siichukulii kama taifa mshirika, lakini kama adui ya nchi yangu," alinukuliwa akisema katika barua hiyo, ambayo iliwekwa saini na Bw Nkurunziza mnamo tarehe 4 Desemba.

Kiongozi huyo aliitisha kikao maalum cha EAC kufanyika ili kujadili mzozo huo kati ya Rwanda na Burundi.

Burundi inasisitiza kwamba Rwanda ndiyo chanzo kikuu cha machafuko yaliyotokea Burundi tangu Aprili 2015 na kwamba mzozo huo ulianza mapema mwaka 2010 wakati baadhi ya makundi ya upinzani yalipoanza kusema kwamba hakungekuwa na uchaguzi 2015.

Haki miliki ya picha Getty Images

Burundi inadai kwamba Rwanda imekuwa ikihusika katika visa vya utovu wa amani nchini mwake, ikishirikiana na mkoloni wa zamani Ubelgiji.

"Rwanda ilikataa kushirikiana na kundi la pamoja la kutathmini hali halisi lakini Burundi ilishirikiana kikamilifu na huu ni ushahidi tosha kwamba taifa hilo halijawahi kutaka ukweli ufahamike kwa sababu ya uchochezi wake dhidi ya Burundi.

"Ni wazi kwamba Jumuiya ya Afrika Mashariki haifai kufumbia macho mateso haya yanayowakuta wana wa Burundi."

Vilevile Burundi imesema kamwe haitakubali pendekezo la jumuiya ya kimataifa la kuruhusu vikosi kutoka nje kudumisha amani Burundi na kutolewa kwa msamaha kwa wanaodaiwa kuhusika katika jaribio la mapinduzi ya serikali ya mwaka 2015 kama masharti kabla ya kufanyika kwa uchaguzi wa mwaka 2020.

Burundi imekuwa ikikanusha kuyaunga mkono makundi ya waasi dhidi ya Rwanda.

Nchi hizo mbili zimekuwa katika mgogoro tangu mwezi Aprili mwaka 2015 wakati serikali ya Burundi ilipoishutumu Rwanda kuunga mkono jaribio lililoshindwa dhidi ya Raisi Pierre Nkurunziza

Mahusiano yao hayajarejea kama kawaida tangu wakati huo, kuna hofu kuwa mvutano uliopo unaweza kuwa sababu ya mashambulizi ya hivi sasa kwa nchi zote mbili dhidi ya maeneo ya jeshi.